iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Usafi_wa_moyo
Usafi wa moyo - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Usafi wa moyo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa Domenichino unaodokeza usafi wa moyo.

Usafi wa moyo (kwa Kiingereza: chastity, kutoka Kilatini: castitas) ni neno lilivyotumiwa na Yesu katika Hotuba ya mlimani kwa maana pana kabisa na inayohusisha unyofu wa dhamiri kwa jumla.

Hata hivyo, neno hilo linatumika mara nyingi, hasa katika Kanisa Katoliki[1][2][3], kuelezea adili ambalo linapingana na uzinifu na kutegemea kiasi na ambalo linasisitizwa sana na Biblia na Kurani. Kwa maana hiyo unawahusu watu wanaojua kutawala maelekeo ya kijinsia yaweze kujenga maisha yao binafsi, familia na hata jamii.

Hapa tutazingatia usafi wa moyo kama aina muhimu zaidi ya adili la kiasi, kwanza kwa jumla, unavyotakiwa katika hali yoyote ya maisha, hata katika ndoa. Halafu tutaona unavyozaa Kiroho, hasa ukitekelezwa kwa namna bora, yaani katika ubikira. Juu yake, Yesu alisema, “Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee” (Math 19:12). Mtaguso wa Trento umetamka rasmi kwamba hali ya useja mtakatifu ni bora kuliko ile ya ndoa, kama Mtume Paulo alivyofundisha wazi katika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho 7:25,38,40.

Lengo la usafi wa moyo

[hariri | hariri chanzo]

Ingawa haya inastahili sifa, si adili bali elekeo jema la umbile tu. Kumbe usafi wa moyo ni adili linaloingiza mwanga wa akili nyofu na wa neema katika hisi zinazovurugika. Ubikira ni adili kubwa zaidi kwa kuwa unamtolea Mungu utimilifu wa mwili na moyo na kumwekea wakfu maisha yote; ni zawadi azizi ambayo inalitia Kanisa uangavu wa pekee na kulipamba kwa sifa ya utakatifu.

Tunaona thamani ya usafi wa moyo (katika ndoa pia) hasa tukifikiria vurugu ambazo zinatokana na tamaa za mwili, na kusababisha hata talaka, aibu kwa familia nzima, utovu wa raha kwa wanandoa na kwa watoto wao. Ili kutukinga nazo, Bwana alisema, “Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe… Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika Jehanum” (Math 5:29-30). Usafi unapotezwa kwa hisi, kwa mawazo, kwa tamaa. Haukubali aina yoyote ya ashiki iliyokatazwa; kinyume chake unapunguza hata zile halali ambazo hazihitajiki: unatuelekeza kutoambatana nazo. “Kukwepa hasira ni rahisi kuliko kuiratibu; vivyo hivyo kujinyima kabisa ashiki ni rahisi kuliko kuwa na kiasi ndani yake” (Fransisko wa Sales).

Lengo lake liwe upendo wa Mungu, kwa kuwa usafi wa moyo na wa mwili ni kujinyima mapenzi yoyote haramu kwa ajili yake. Unazuia maisha ya moyo yasiteremke, ili yaweze kuinuka kwa Mungu kama mwali hai na safi wa moto mkali zaidi na zaidi. Usafi wa viungo ni kama ganda la ule wa moyo ambao ndio wa thamani zaidi. Hauwezekani pasipo aina mbili za ufishaji: ule wa mwili na hisi, hasa mbele ya hatari, na ule wa moyo, unaojikatalia mapenzi yoyote yasiyoratibiwa: hayo yana madhara na utelezi kwenye mteremko wa kutisha. Kasi ya kwenda chini inaweza ikaongezeka kuliko tulivyodhani, halafu kupanda juu tena ni kugumu. Mara nyingi mtu anajitengenezea minyororo ambayo baadaye hana moyo wa kuivunja. Ulimwengu ukisema, “Mapenzi ya kibinadamu yana haki zake”, tujibu, “Hayataweza kamwe kuwa na haki dhidi ya upendo wa Mungu, aliye wema mkuu na asili ya mapenzi yoyote halali”.

Ili tudumishe adili hilo tunapaswa kuambatana daima na Yesu msulubiwa. “Mtu anapoanza kutamani kitu pasipo utaratibu, mara anakosa utulivu… Amani halisi ya moyo inapatikana kwa kupinga maono, si kwa kuyafuata. Amani hiyo ni tuzo la mtu mwenye juhudi na maisha ya Kiroho… Anayepotewa na Yesu anapata hasara kubwa kuliko kama angepoteza ulimwengu wote. Anayempata, amevumbua hazina isiyo na mwisho, kuu kuliko mema yote… Pendeni marafiki na maadui ndani mwake na kwa ajili yake, na kumuomba kwa ajili ya wote ili wamjue na kumpenda” (Kumfuasa Yesu Kristo I,6:1-2; II,8:2-4). “Yesu, tumaini la wanaotubu, / jinsi ulivyo mpole kwa waombao! / Jinsi ulivyo mwema kwa wanaokutafuta! / Lakini hasa u nini kwa wanaokupata!” (Utenzi wa Jina takatifu la Yesu). Ili tuufikie urafiki huo wa ndani na Kristo, ni lazima tutekeleze mfululizo unyenyekevu na usafi wa moyo pasipo kuyataja kamwe au kwa nadra tu.

Adili hilo linavyozaa Kiroho

[hariri | hariri chanzo]

Usafi kamili unatufanya tuishi mwilini kwa namna ya Kiroho iliyo utangulizi wa uzima wa milele. Kwa namna fulani unatufanya tufanane na malaika na kuwa huru kuhusu vyote vinavyoonekana. Tena unafanya mwili uzidi kufanana na roho, na roho izidi kufanana na Mungu.

Mwili ukiishi kwa ajili ya roho tu, unaelekea kufanana nayo. Roho si ya kimwili, inaonekana na Mungu na malaika tu; ni sahili kwa kuwa haina sehemu; ni nzuri kama mawazo na matendo maadilifu, hasa ikiwa na nia njema daima; ni tulivu maana haipatwi na badiliko lolote la mwili; haiharibiki kwa sababu haitegemei mwili unaokufa. Basi, kwa usafi, mwili pia, kwa namna fulani, unakuwa wa Kiroho na kuruhusu roho ionekane kwa njia yake, hasa katika macho: yale ya mtakatifu yanaonyesha nini? Kwa adili hilo mwili unakuwa sahili: mwenendo wa kahaba una fujo, ule wa bikira ni sahili. Kutokana na usafi, mwili unakuwa mzuri, kwa sababu kila kilicho safi ni kizuri, kama anga lisilo na mawingu na kama almasi inayopitisha mwanga. Kwa usafi mwili unakuwa mtulivu: vilema vinauharibu kabla ya wakati, kumbe ubikira unautunza. Miili ya Bwana na ya bikira Maria haikuoza kaburini, na mara kadhaa masalia ya watakatifu hayaozi, hata kwa muda fulani yanaendelea kunukia.

Ikiwa ni kweli kwamba usafi kamili unaufanya mwili ufanane na roho, ni kweli zaidi kwamba unaifanya roho ifanane na Mungu. Sifa tatu maalumu za Nafsi za Kimungu ni uweza, hekima na upendo. Basi, kwa usafi kamili roho inazidi kuwa na nguvu, mwanga na upendo. Ndipo panapoonekana hasa adili hilo linavyozaa matunda. Usafi kamili unampatia sista nguvu na mamlaka hospitalini au magerezani, hata mara nyingi akaheshimiwa na watu wapotovu! Hasa bikira Maria ni tishio la mashetani!

Kwa usafi roho inaangazwa: “Heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu” (Math 5:8). Kati ya Wainjili, tai alikuwa na usafi kamili, na vilevile Mtume Paulo. Mwanateolojia bora, Thoma wa Akwino, alipokuwa na umri wa miaka kumi na sita aliondolewa moja kwa moja vishawishi vya uzinifu aweze kuzama katika mafumbo ili awashirikishe wengine. Pengine usafi kamili unawapa watakatifu uwezo upitao maumbile wa kuona kwa namna fulani uzuri wa Mungu na ulinganifu wa sifa zake zinazoonekana kupingana; hata pasipo elimu, wanaandika maneno yasiyosahaulika.

Hatimaye, usafi kamili unaitia roho upendo kwa Mungu na kwa jirani ambao ni mara mia kweli na unatuza kwa ziada sadaka zote unazozidai. Katika moyo safi upendo unazidi kuwa mtamu na wa nguvu. Mbali na mabubujiko ya mapenzi ya juujuu, unainuka juu ya hisi na kuwa mwali hai katika utashi. Chini ya Roho Mtakatifu, moyo unaungana na ule wa Mwokozi ili kuchota ndani mwake nguvu kubwa zaidi na zaidi na uhai mpya daima. Upendo huo unaonjesha uzima wa milele.

Roho iliyowekwa wakfu kwa Mungu, ikiwa aminifu moja kwa moja, inastahili kuitwa bibi arusi wa Kristo, kwa kuwa upendo unaishirikisha huzuni na furaha za Yesu, kazi yake kwa ajili ya watu na ushindi wake. Kwenye kilele cha mpando huo kuna arusi ya roho na Mungu wake. Ni muungano usiovunjika unaomgeuza mtu ndani ya Mungu hata anaweza kusema, “Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake” (Wim 2:16). Ni uelewano wa ndani unaofikia hatua ya kufunua mawazo ya siri zaidi: bibi arusi wa Kristo anayahisi mambo mengi kabla ya wakati. Ni ushirika kamili wa mawazo, mapenzi, matakwa, sadaka na matendo kwa wokovu wa watu: ushuhuda wake ni Komunyo ya kila siku ikizidi kuwa motomoto (upande wa utashi, hata kama si upande wa hisi).

Upendo safi na wa nguvu hivyo ni chanzo cha ubaba au umama wa Kiroho. Kama vile Yesu alivyowaambia mitume, “Enyi watoto wadogo…” (Yoh 13:33), nao waliwaandikia wanafunzi wao, “Watoto wangu wadogo…” (1Yoh 2:1). “Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu!” (Gal 4:19). “Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?” (2Kor 11:29). Ndio ubaba wa Kiroho katika ukarimu, hisani na nguvu zake zote, uliofidia kwa ziada ubaba wa kimaumbile waliojinyima. Badala ya kuanzisha kaya ili kueneza uhai wa kibinadamu, walimzalia Bwana watu ambao waishi milele. Tupendezwe vilevile na umama wa Kiroho wa masista kwa watu wenye shida za kila aina; wataambiwa, “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Math 25:40). Ndivyo tunavyoona ukuu wa shauri hilo la Kiinjili. Pengine roho ya shauri hilo iligeuza hata ubaba au umama wa kimaumbile, k.mf. Monika aliyemzaa upya mwanae Augustino kwa machozi na sala.

Katika hayo yote tunaona jinsi adili la usafi wa moyo, likieleweka na kutekelezwa sawasawa, linavyoandaa kumiminiwa sala ambapo ahadi ya kumuona Mungu inaanza kutimia. Kwa moyo safi tunaanza kumuona kwa namna fulani katika sala, katika ekaristi, katika maongozi ya maisha ambayo “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema” (Rom 8:28), na hatimaye katika wale wanaotuzunguka, ambao pengine tunakuja kutambua kwamba wanampendeza Bwana kuliko tulivyodhani, ingawa kwa nje hawapendezi. Lakini mwanga huo unapatikana polepole tu kwa kujikana na kumpenda kwa usafi na nguvu kubwa zaidi na zaidi.

  1. (Kilatini) Sextum Praeceptum (Katekisimu ya Kanisa Katoliki)
  2. (Kiitalia) Castitas Archived 12 Oktoba 2007 at the Wayback Machine. Usafi wa moyo katika Biblia na katika Ualimu wa Kanisa
  3. (Kiitalia) Orientamenti educativi sull'amore umano. Kwa lugha nyingine nne, ikiwemo ile ya Kiingereza: Congregazione per l'Educazione Cattolica

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]