iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Pointe-Noire
Pointe-Noire - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Pointe-Noire

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pointe Noire

Pointe-Noire (kwa Kikongo: Ninji) ni mji mkubwa wa pili katika Jamhuri ya Kongo, kufuatia mji mkuu wa Brazzaville. Jiji hili huwa na hadhi ya mkoa tangu mwaka 2004. Kabla ya tarehe hiyo ilikuwa makao makuu wa mkoa wa Kouilou.

Mji ulianzishwa kwenye rasi ndogo katika Bahari ya Atlantiki. Pointe-Noire ni kitovu kikuu cha biashara nchini ikiwa na wakazi 715,334 (2007). [1] Rundiko la mji lina wakazi zaidi ya milioni moja.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Jina la Pointe-Noire linamaanisha kwa Kifaransa "nukta nyeusi" likitokana na mabaharia Wareno walioona huko mnamo mwaka 1484 miamba mieusi kwenye rasi ndogo. Wakachora alama hiyo kwenye ramani wakaiita Ponta Negra kwa Kireno. Kuanzia wakati huo na kuendelea, Pointe-Noire, iliyoitwa kwa Kireno Ponta Negra, ikawa mahali pa kumbukumbu kwa wanamaji waliopita huko. Mnamo 1883 Wafaransa walifanya mkataba na ufalme wa Loango na kuanzisha kituo cha uvuvi hapo walichokiita "Pointe-Noire".

Mnamo mwaka wa 1910 koloni la Afrika ya Ikweta ya Kifaransa (Afrique équatoriale française, AEF) liliundwa na Wafaransa wakilenga kufaidika na utajiri wa Kongo. Hapo walihitaji reli kutoka Brazzaville hadi pwani ya Atlantiki wakachagua Pointe-Noire kama mahali panapofaa kuanzisha bandari.[2]

Mnamo 1927 mji ulikuwa na wakazi 3,000 tayari ukapata mfumo wa maji ya bomba. Uwanja wa ndege ulijengwa mnamo 1932. Mnamo 1934, Gavana Raphael Antonetti alizindua Reli ya Kongo-Bahari. Hospitali ya kwanza ilijengwa mnamo 1936. Mwaka huohuo, Benki ya Afrika Magharibi (BAO) ilifungua tawi lake la kwanza jijini. Mnamo 1942, bandari ya Pointe-Noire ilikaribisha meli yake ya kwanza.

Mnamo 1950, Pointe-Noire ilikuwa na wakazi 20,000, ikawa mji mkuu wa "Kongo ya Kati", wakati Brazzaville ilikuwa mji mkuu wa Afrika ya Ikweta ya Kifaransa. Mnamo 1957, Kongo ya Kati ikawa Jamhuri ya Kongo, ingawa haikuwa huru bado.

Matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa wabunge wa mwaka 1958 yalisababisha viongozi wa Muungano wa Kidemokrasia wa Kutetea Maslahi ya Kiafrika (Union démocratique pour la défense des interets africains, UDDIA) kuhamisha mji mkuu hadi Brazzaville, kwa kuwa Pointe-Noire ilikuwa chini ya ushawishi wa upinzani wa kisiasa.

Wakati wa uhuru mwaka 1960 Pointe-Noire ilikuwa mji wa nchi ulioendelea zaidi.

Tangu mwaka 1980 mafuta yaligunduliwa baharini karibu na pwani na Pointe-Noire iliendelea kuwa kitovu cha tasnia ya mafuta. Idadi ya wakazi ikaongezeka haraka ikafikia 360,000 mnamo 1994.

Mapigano ya vita ya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 1997 na 1999 yalisababisha mawimbi ya wakimbizi kutoka mikoa jirani kuelekea Pointe-Noire, na kusababisha idadi ya watu kupanda hadi zaidi ya wakazi milioni 1.

Mbao za kuuza nje katika Bandari ya Pointe-Noire

Pointe-Noire ni kituo muhimu cha sekta ya mafuta ya Jamhuri ya Kongo, ambayo ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa mafuta katika Afrika ya Kati. Mafuta ya Kongo yametolewa hasa na kampuni ya Kifaransa ya Elf Aquitaine tangu kugunduliwa kwake karibu 1980.

Pointe-Noire pia inajulikana kwa tasnia yake ya uvuvi, ambayo mara nyingi haikubaliani na ukuzaji wa mafuta. [3] Maji ya eneo hilo yanaripotiwa kuvuliwa kupita kiasi. [4]

Pointe-Noire ni nyumbani kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Agostinho-Neto ambao kufikia Mei 2015 ulikuwa na safari za ndege za moja kwa moja hadi Abidjan, Addis Ababa, Brazzaville, Casablanca, Cotonou, Douala, Kinshasa–N'Djili, Libreville, Lomé, Malabo, Paris–Charles de Gaulle, Port-Gentil, na Johannesburg–OR Tambo na ulikuwa uwanja wa ndege wa pili nchini kwa idadi ya ndege zilizotua na kuondoka. Pointe-Noire pia ni kituo cha Reli ya Kongo-Bahari, kituo cha reli kikiwa jengo mashuhuri. Mnamo mwaka 2014 reli hiyo ilikuwa ikiendesha huduma ya treni ya La Gazelle kila siku ya pili hadi Brazzaville. [5]

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Administrator. "Population des Départements". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 14 Novemba 2018. Iliwekwa mnamo 24 Mei 2016.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. John Frank Clark, Samuel Decalo, Historical Dictionary of Republic of the Congo, Scarecrow Press, USA, 2012, p. 365
  3. Tati, Gabriel (2004). "Sharing Public Space in Pointe-Noire, Congo-Brazzaville: Immigrant Fishermen and a Multinational Oil Company". Katika Hansen, Karen Tranberg (mhr.). Reconsidering informality: perspectives from urban Africa. Nordic Africa Institute, 2004. ku. 235. ISBN 91-7106-518-0.
  4. "The rise of shark fishing off the Congolese coast", Al Jazeera, 22 November 2021 https://www.aljazeera.com/gallery/2021/11/22/in-pictures-sharks-and-artisanal-fishermen-struggle-to-survive
  5. 2014 Timetable, Lonely Planet, https://www.lonelyplanet.com/thorntree/forums/africa/congo/la-gazelle-train-brazzaville-to-pointe-noire