iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Mnara_wa_taa
Mnara wa taa - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Mnara wa taa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mnara wa taa nchini India.
Mnara wa taa mwishoni mwa ulimwengu huko Ushuaia, Argentina
Mnara wa taa kati ya bahari.

Mnara wa taa ni mnara au jengo refu kando ya bahari lenye taa kubwa juu yake. Kusudi lake ni kupatia meli baharini mwongozo wakati wa usiku. Nuru yake huonyesha njia ya kufika bandarini, pia ni onyo la kwamba pwani iko karibu.

Siku hizi minara ina urefu kati ya mita 15 hadi 40. Kama mnara umejengwa mwambaoni juu ya jabali unaweza kuwa mfupi zaidi maadamu nuru yake inaonekana bila matatizo.

Kichoro cha Pharos ya Aleksandria.

Minara ya taa ya kwanza

Minara ya taa ya kwanza ilikuwa na moto juu yake na nuru ya moto ilionekana mbali. Mnara wa kwanza unaojulikana vizuri kihistoria ulikuwa Pharos ya Aleksandria nchini Misri uliyojengwa mnamo mwaka 282 KK. Ulisimama hadi mwaka 1303 BK ulipobomolewa na tetemeko la ardhi. Umekadiriwa kuwa na urefu wa mita 115 hadi 160. Wagiriki wa Kale waliuhesabu kati ya maajabu saba ya dunia.

Mabadiliko ya teknolojia

Maendeleo ya teknolojia yaliona taa za mafuta kuchukua nafasi ya moto halafu taa za gesi kutumiwa badala ya mafuta. Siku hizi taa zote ni za umeme. Taa hizo zinazunguka ndani ya chumba cha juu cha mnara na lenzi zinaongeza ukali wa mwanga.

Mitambo ya GPS kwenye meli kubwa imepunguza haja ya kuwa na minara ya taa lakini hadi leo ni muhimu kwa ajili ya usalama kama mitambo inakwama.

Zamani kila mnara ulikuwa na mlinzi wake aliyeangalia moto au taa. Siku hizi taa zinafanya kazi peke yake zikisimamiwa na tarakilishi.