iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Mbwa_Mdogo_(kundinyota)
Mbwa Mdogo (kundinyota) - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Mbwa Mdogo (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Mbwa Mdogo (Canis Minor) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Mbwa Mdogo - Canis Minor jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini

Mbwa Mdogo (kwa Kilatini na Kiingereza Canis Minor) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakaskazi ya Dunia.

Mahali pake

Mbwa Mdogo - Canis Minor lipo angani si mbali na nyota angavu sana ya Shira (Sirius). Linapakana na kundinyota jirani za Mapacha) (pia Jauza, lat. Gemini), Kaa (pia Saratani, lat. Cancer), Shuja (Hydra) na Monukero (Monoceros). Haipakani moja kwa moja na Mbwa Mkubwa (Canis Major).

Jina

Mbwa Mdogo (Canis Minor) halikujulikana kwa mabaharia Waswahili kama kundinyota ya pekee[2]. Waarabu waliijua kwa jina la الكلب المتقدّم al-kalb al-mutaqaddim kwa maana “mbwa wa kutangulia” na hapa walitafsiri jina la Kigiriki liliopatikana kwa Ptolemaio aliyetaja nyota kuu kwa jina la Πρκυον prokion kwa maana ileile [3] . Wagiriki waliiona nyota ya Alfa Canis Minoris jinsi ilivyotangulia kuonekana angani kabla ya Shira (Sirius) au “Mbwa Mkubwa”.

Kwa hiyo hata Wagiriki hawakuangalia hapa kundinyota lakini walijali tu nyota yake ya Alfa au Procyon. [4].

Canis Minor - Mbwa Mdogo ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika kitabu cha Almagesti wakati wa karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [5] kwa jina la Canis Minor. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'CMi'.[6]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Alfa Canis Minoris au Procyon [7]. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 0.34 ikiwa umbali wa miakanuru 11.4 kutoka Dunia yetu[8][9].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
α 10 Procyon 0,40m 11,4 F5 IV
β 3 Gomeisa 2,89m 150 B8 V
γ 4 4,33m 200 K3 III
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Canis Minor" katika lugha ya Kilatini ni "Canis Minoris" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Canis Minoris, nk.
  2. Haiko katika orodha za Knappert, wala nyota ya Procyon.
  3. PAL - Glossary Tri", tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. Linganisha Allen uk. 132
  5. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  6. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  7. CMi-Procyon - Naming Stars, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Novemba 2017
  8. Canis Minor, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  9. Procyon (Alpha Canis Minoris), tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 131 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331