iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Inter-territorial_Language_(Swahili)_committee
Inter-territorial Language (Swahili) committee - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Inter-territorial Language (Swahili) committee

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Inter-territorial Language (Swahili) committee (Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili) ni mtangulizi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Daressalaam.

Sababu za kuundwa kwa kamati

[hariri | hariri chanzo]

Iliundwa mwaka 1930 kama kamati yenye shabaha ya kuunda na kuendeleza Kiswahili sanifu katika maeneo ya Afrika ya Mashariki yaliyokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza yaani Kenya, Tanganyika, Zanzibar na Uganda. Kati ya maeneo haya Kenya ilikuwa koloni, Uganda na Zanzibar zilikuwa nchi lindwa na Tanganyika ilikuwa eneo la kukabidhiwa chini ya uangalizi wa Shirikisho la Mataifa. Hivyo Waingereza walizoea kuyataja kwa jumla kama "East African dependencies" au "East African territories" yaani maeneo ya Afrika ya Mashariki.

Katika maeneo haya Waingereza walianza tayari kutumia Kiswahili kwa ngazi mbalimbali ya utawala wao. Walikuwa wamekuta lugha hii kama chombo cha mawasiliano kwenye pwani na pia kwenye njia za misafara hadi ziwa Viktoria. Katika Tanganyika iliyowahi kutawaliwa na Ujerumani kama Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hadi 1918 Kiswahili ilikuwa lugha rasmi ya utawala kwenye ngazi za chini. Sehemu ya shule za misioni zilitumia Kiswahili kama lugha ya kufundisha badala ya lugha za kikabila. Sehemu za Biblia ziliwahi kutafsiriwa lakini na wamisionari mbalimbali waliofuata lahaja tofauti za Kiswahili.

Matatizo ya lahaja na tahajia

[hariri | hariri chanzo]

Tatizo kwa utawala ilikuwa ya kwamba Kiswahili kilipatikana katika lahaja nyingi. Hasa swali la tahajia lilikuwa halieleweki vema kwa sababu Kiswahili asilia kiliandikwa kwa herufi za Kiarabu. Badiliko la kutumia alfabeti ya Kilatini badala ya Kiarabu likaleta tofauti nyingi katika mwandishi wa Kiswahili.

Hapa magavana Waingereza wa maeneo ya Afrika ya Mashariki waliamua kuanzisha kamati itakayounda lugha sanifu kwa matumizi katika sehemu zote.

Azimio muhimu ya kamati ilikuwa kutumia Kiswahili cha Zanzibar yaani Kiunguja kama msingi wa usafinishaji wa lugha.

Kazi ya kamati tangu 1930

[hariri | hariri chanzo]

Kamati hii ilianza kazi yake mwaka 1930 huko Dar es Salaam. Katibu mkuu wa kwanza alikuwa Frederick Johnson akisaidiana na wanakamati wengine kati yao R.K. Watts, P.Mzaba na Seyyid Majid Khalid Barghash. Hadi 1938 wanakamati walikuwa Wazungu tu na tangu 1939 Waafrika walipokelewa kama wanakamati halisi.

Baada ya uhuru kamati iliendelea kwa jina la East African Swahili Committee (Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki).

Ofisi ya kamati ilikuwepo Dar es Salaam ikahamia Nairobi mwaka 1943 halafu Makerere mwaka 1952 baadaye kwa muda mfupi kwenda Mombasa. Tangu 1963 ofisi ilirudishwa Dar es Salaam na tangu 1964 ikawa chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa jina la Chuo cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili (Institute of Kiswahili Language Research). Tangu 1970 imekuwa taasisi kamili ya Chuo Kikuu ikijulikana kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na tangu 2009 kama Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).

Kamusi za kamati

[hariri | hariri chanzo]

Kamati ilitoa hasa kamusi mbili za Kiingereza-Kiswahili (M-J SES) na Kiswahili-Kiingereza (M-J SSE) zinazotajwa mara nyingi kwa kifupi "Madan-Johnson" kwa sababu kamusi ya Madan ilikuwa msingi wa kazi ya kamati na Johnson alikuwa mhariri mkuu. Kamusi hizi zatolewa hadi leo hata kama maneno kadhaa ndani yao hayatumiwi tena na maneno mapya yakosekana lakini kwa jumla ni kamusi bora zinazosaidia kuelewa hata Kiswahili cha zamani kidogo.