iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Hilari_wa_Poitiers
Hilari wa Poitiers - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Hilari wa Poitiers

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hilari akiwekwa wakfu kuwa Askofu wa Poitiers.

Hilari wa Poitiers (315 hivi - 367), askofu wa mji huo (kwa Kilatini Pictavium), Galia, leo Ufaransa), mwanateolojia, mwanafalsafa na mwandishi.

Alichangia teolojia, k. mf. kuhusu Ufunuo, akiunganisha mitazamo ya Kikristo ya mashariki na ya magharibi.

Tangu zamani anaheshimiwa na Kanisa Katoliki, Waorthodoksi, halafu na Waanglikana kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Wakatoliki wanamheshimu pia kama mwalimu wa Kanisa tangu mwaka 1851, alipotangazwa na Papa Pius IX.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Januari[1].

Hilari akizaliwa mwaka 315 hivi katika familia ya kisharifu, lakini si ya Kikristo.

Maandishi yake yanaonesha alipata elimu nzuri kuhusu fasihi, akavutiwa mapema na falsafa na kutafuta ukweli.

Akitafakari hatima ya binadamu na kusoma Biblia, hatimaye aliongokea Ukristo akabatizwa mwaka 345 hivi.

Alikuwa baba wa nyumbani alipochaguliwa askofu wa Poitiers mwaka 353.

Mwaka 354 tu alikuja kujua Kanuni ya Imani ya Nisea, akaanza kuitetea katika sinodi na mitaguso dhidi ya uzushi wa Ario.

Kwa ajili hiyo mwaka 356 kwa ombi la maaskofu Waario alipelekwa na Kaisari Konstans II uhamishoni Frigia (leo katika Uturuki).

Akiishi huko miaka minne iliyofuata alipata nafasi ya kuchimba mafundisho ya mababu wa Kanisa wa mashariki, hata akaanza kuandika juu ya Utatu (De Trinitate).

Humo anasimulia safari yake kuelekea imani ambayo aliiungama katika ubatizo akiwa tayari kuishika daima na hata kuifia. Hilari anajenga teolojia yake juu ya maneno ya kubatizia yaliyoagizwa na Yesu, akisisitiza ukweli wa majina “Baba” na “Mwana” yanayomaanisha kuwa dhati yao ni moja.

Anajitahidi kuonyesha sehemu mbalimbali za Agano la Kale ambazo pia zinadokeza umungu wa Mwana na usawa wake na Baba. Kuhusu sehemu za Agano Jipya zinazoweza kuleta utata, anafundisha kutofautisha zile zinazosema juu ya Yesu kama Mungu na zile zinazosema juu yake kama mtu.

Aliandika: “Mungu hajui kuwa chochote ila upendo, hajui kuwa yeyote ila Baba. Wenye upendo hawana kijicho, na yule ambaye ni Baba ni hivyo kikamilifu”. Kwa sababu hiyo Mwana ni Mungu kweli pasipo upungufu wowote. “Yule anayetokana na aliye mkamilifu ni mkamilifu vilevile kwa sababu yeye ana yote, ametoa yote”.

Binadamu wanapata wokovu kwa Kristo tu, Mwana wa Mungu na Mwana wa Adamu, ambaye kwa kujifanya mtu ameunganika na watu wote. “Kwa kuhusiana na mwili wake, wote wanaweza kumfikia Kristo, mradi wavue nafsi yao ya awali kwa kuipigilia msalabani; mradi tunaachana na maisha yetu ya kwanza na kuongoka ili tuzikwe pamoja naye katika ubatizo wake tukitarajia uzima”.

Huko uhamishoni aliandika pia Kitabu cha Sinodi ambamo kwa faida ya maaskofu wenzake wa Galia, alikusanya na kufafanua maungamo ya imani na hati nyingine za sinodi za mashariki za wakati ule.

Kabla na baada ya vitabu hivyo, aliandika ufafanuzi wa Zaburi na sehemu nyingine za Biblia kuanzia Injili ya Mathayo, mbali ya tenzi za dini na vitabu vya historia. Kati ya maandishi yake yote, mengi yametufikia.

Kuhusu Zaburi, alizifafanua kwa mtazamo huu: “Bila shaka mambo yote yanayosemwa katika Zaburi yanatakiwa kueleweka kadiri ya tangazo la Injili, hivi kwamba, haidhuru roho ya unabii imesema kwa sauti gani, yote yaweze kuhusianishwa na ujuzi wa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo, wa umwilisho, mateso na ufalme, na uwezo na utukufu wa ufufuko wake”. Hivyo katika Zaburi zote aliona fumbo la Kristo na la mwili wake, yaani Kanisa.

Aliporuhusiwa kurudi kwao aliwajibika tena katika uchungaji wa jimbo lake, lakini aliathiri Kanisa hata nje ya mipaka yake hasa kwa mafundisho yake; hivyo alikuwa mhusika mkuu wa Mtaguso wa Paris (361) uliotumia misamiati ya Mtaguso I wa Nisea, na kwa kutumia nguvu na busara pamoja, alifaulu kurudisha Waario wengi katika Kanisa na kueneza Ukristo.

Kutokana na juhudi zake aliitwa “Atanasi wa magharibi”.

Kati ya wanafunzi wake muhimu zaidi, yupo Martin wa Tours, aliyeanzisha monasteri karibu na Poitiers halafu akawa askofu mmonaki wa kwanza katika Kanisa la Magharibi.

Alifariki mwaka 367.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Mungu, Baba Mwenyezi, najua vema kuwa huduma kuu inayonipasa kwako katika maisha yangu ni kwamba kila neno na wazo langu liseme juu yako.

Kipawa cha kusema ulichonijalia hakiwezi kunipa furaha kubwa kuliko ile ya kukutumikia kwa kuhubiri na kuonyesha kwa ulimwengu usiokujua, au kwa mzushi anayekukanusha, jinsi ulivyo, yaani Baba, Baba ambaye Mwanae pekee ni Mungu.

Lakini kwa kusema haya, nasema tu ninachotaka kufanya. Ili niweze kukifanya kweli nahitaji kuomba msaada wako na huruma yako, kuomba ujaze upepo tanga nilizozipandisha kwa ajili yako na uzisukume mbele katika mwendo wangu, yaani umvuvie Roho wako katika imani yangu na katika kuiungama, na uniwezeshe kuendelea mahubiri niliyoyaanza…

Acha niseme nawe, Mwenyezi Mungu, ingawa ni mavumbi na majivu tu, acha niseme kwa uhuru kwa kuwa nimefungamana nawe kwa vifungo vya upendo.

Kabla sijakufahamu nilikuwa si kitu. Nilikuwa na bahati mbaya ya kutojua maana ya maisha, nilikuwa sijielewi, nilikuwa tofauti kabisa na jinsi nilivyo. Huruma yako ndiyo iliyonipa uhai…

Muda wote ambao nitaishi na kupumua kwa pumzi uliyonipa, Baba Mtakatifu, Mwenyezi Mungu, nitakiri kwamba tangu milele yote wewe si Mungu tu, bali Baba pia.

Sitakuwa kamwe na kichaa na uovu wa kujifanya hakimu wa uwezo wako usio na mipaka, wala wa mafumbo yako, hata nipendelee wazo langu maskini kuliko yale ambayo dini inakiri juu ya ukuu wako usio na mipaka au imani inafundisha kuhusu umilele wake…

Nakuomba, utunze salama imani hiyo uliyonijalia, na kunifadhilia kwamba muda wote wa maisha yangu niweze tu kuzingatia yale ambayo dhamiri yangu inasema juu yake.

Niweze daima kushika imani niliyoiungama nilipozaliwa upya, Nishike ungamo lake nililolitamka nilipobatizwa kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu.

Niweze kukuabudu wewe, Baba yetu, na kumuabudu Mwanao pamoja nawe; niweze kuwa jinsi Roho wako Mtakatifu anavyotaka niwe, yeye atokaye kwako kwa njia ya Mwanao pekee.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Maandishi

[hariri | hariri chanzo]
Lucubrationes, 1523
  • De Trinitate ndio kitabu chake bora; kilikuwa cha pekee katika Kilatini
  • Tenzi
  • Contra Arianos vel Auxentium Mediolanensem liber
  • Contra Constantium Augustum liber
  • Commentarius in Evangelium Matthaei
  • Tractatus super Psalmos

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]