iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Dario_I
Dario I - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Dario I

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa Dario.

Dario Mkuu (pia Dario I, mnamo 549 KK486/485 KK) alikuwa mtawala wa Uajemi ya Kale (leo Iran) kuanzia 522 KK hadi 485 KK. Hutazamwa kama mfalme wa tisa katika nasaba ya Waakhameni.

Pamoja na Koreshi Mkuu, Dario hutazamwa kama mfalme mkuu wa Uajemi ya Kale aliyefaulu sana. Alipanga utawala kwa namna iliyoongeza nguvu ya milki yake. Aligawa milki yote katika majimbo ishirini na kuweka gavana juu ya kila eneo. Alianzisha sarafu za dhahabu na kuendeleza biashara ndani ya himaya yake na kufanya biashara ya nje.

Dario aliwaruhusu Wayahudi kujenga upya Hekalu la Yerusalemu. Kuhusiana na hilo, anatajwa katika Biblia ya Kiebrania, hususan katika vitabu vya Hagai, Zekaria, Ezra na Nehemia.

Pia alijenga mahekalu mengi huko Misri. Ujenzi mkubwa zaidi ambao ulitekelezwa na Dario ulikuwa mji mkuu mpya wa Persepolis, karibu na Pasargadae.

Dario aliaga dunia huko Persepolis. Kaburi lake lilikatwa kwenye mwamba karibu na Persepolis. Baada ya kifo chake, Xerxes akawa Shah wa Iran.

Vyanzo vya kihistoria

[hariri | hariri chanzo]

Dario aliacha maandiko kadhaa yaliyokatwa katika mwamba na kuhifadhiwa hadi leo. Kwenye mlima wa Behistun kuna matini ya Dario anapoeleza ukoo wake na jinsi alivyompindua mfalme aliyemtangulia anayemtaja kama tapeli. Chini ya jiwe la msingi la ukumbi mkubwa wa Persepolis sanduku lenye kurasa za bati la dhahabu lilikutwa ambamo Dario alieleza ukubwa wa milki yake, kutoka Uhindi hadi Ugiriki na kutoka Sogdia (Tajikistan ya leo) hadi Kushi (Sudani au Ethiopia ya leo).[1]

Mwanahistoria wa Ugiriki ya Kale, Herodoti, aliyezaliwa wakati wa uhai wa Dario, aliandika mengi juu yake katika vitabu vyake vya historia.

Dario anatajwa mara kadhaa katika vitabu vya Biblia kama vile Ezra 6 penye taarifa kuhusu amri yake ya kutekeleza maagizo ya mfalme Koreishi Mkuu kujenga upya hekalu La Yerusalemu. Anatajwa pia katika kitabu cha nabii Hagai. "Dario Mmedi" anayetajwa katika kitabu cha Danieli mlango wa sita si Dario I.

Familia na asili

[hariri | hariri chanzo]

Dario alikuwa mwana mkubwa wa Hystaspes, Mwajemi kutoka nasaba ya Waakhemi na gavana wa Baktria chini ya mfalme Koreishi Mkuu[2]. Kufuatana na taarifa ya Herodoti, wakati wa vita ya Kambisi II huko Misri, Dario alikuwa mwanajeshi na labda mlinzi wa mfalme [3].

Kuwa mfalme

[hariri | hariri chanzo]

Katika maandishi yaliyomo kwenye mwamba wa Bisotun, Dario alieleza kwamba alikuwa mfalme baada ya kumwua tapeli Gautama. Katika taarifa hiyo mfalme Kambisi alimwua mdogo wake Bardiya kabla ya kuondoka na kuvamia Misri. Lakini kifo cha Bardiya haikujulikana. Wakati wa kutokuwepo kwa mfalme kwao Uajemi, tapeli Gautama alijitangaza kuwa Bardiya mdogo wa mfalme aliyeongoza uasi ilhali Kambisi alifariki dunia baada ya kujeruhiwa kwenye safari ya kurudi. Pamoja na wasaidizi wachache, Dario alimwendea katika ngome alipokaa akamwua na kuwa mfalme. [4]. Kimsingi historia ya Herodoti inathibitisha habari hizo.

Wataalamu mbalimbali wana shaka kuhusu ukweli wa simulizi hilo wakiamini kwamba Bardiya hakuuawa na Kambisi; aliasi mwenyewe na kuchukua utawala. Wakosoaji wa taarifa rasmi ya zamani hawataki kuamini kwamba iliwezekana mtu tofauti kuchukua nafasi ya mdogo wa mfalme bila kutambuliwa. Dario aliyemwua alitunga hadithi ya tapeli kwa sababu yeye mwenyewe hakuzaliwa katika familia ya kifalme ila katika tawi la mbali kiasi la nasaba ya Waakhameni. [5].

Kupanua milki

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuwa mfalme, Dario alipaswa kupambana na magavana na watawala wadogo kadhaa waliokataa kumtambua.

Uasi mkubwa ulitokea mwaka 522 KK huko Mesopotamia ambako mtu wa Babeli alijitangaza kuwa mfalme akifuatwa pia na miji mingine; kwa pamoja walitaka kumaliza utawala wa Kiajemi. Dario alishinda jeshi la Wababeli katika mapigano mawili na kurudisha utawala wa Kiajemi.

Baada ya kuimarisha mamlaka yake juu ya himaya yote, Dario alianza kampeni kuelekea Misri ambako alishinda majeshi ya Farao na kuingiza nchi ambazo Kambisi aliwahi kuvamia katika Milki ya Waakhameni.

Mwaka 516 KK, Dario pamoja na jeshi lake aliingia Asia ya Kati hadi Baktria akaendelea akivuka Afghanistan hadi maeneo ya Pakistan ya leo. Mwaka uliofuata alivamia bonde la Mto Indus akathibiti bonde hilo kuanzia Gandhara hadi maeneo ya Karachi ya leo. Alituma kundi la Wagiriki kutoka jeshi lake washuke kwa mashua njia ya Indus hadi Bahari ya Hindi na kupeleleza bahari hiyo hadi Bahari ya Shamu na pwani ya Misri ilhali Dario alirudi Uajemi.

Kaburi la Dario huko Naqsh-e Rostam.

Mnamo 513 KK alishambulia Waskithi upande wa Ulaya. Waskithi walikuwa wafugaji wa farasi, ng'ombe na kondoo waliohamahama katika tambarare upande wa kaskazini wa Bahari Nyeusi, Milima ya Kaukazi na Bahari ya Kaspi hadi Asia ya Kati. Tena na tena makundi yao yalishambulia maeneo ya wakulima na miji upande wa kusini. Mfalme Koreishi Mkuu aliwahi kuuawa katika mapigano dhidi ya Waskithi. Dario aliwafuata hadi Mto Volga akarudi.

Mwaka 490 KK Dario aliamua kuvamia Ugiriki. Sehemu kubwa ya Wagiriki upande wa Asia Ndogo waliishi tayari chini ya utawala wa Kiajemi, na Makedonia katika kaskazini ya Ugiriki ilitambua ukuu wa Dario. Lakini Athens na Sparta ziliendelea kutokubali ubwana wa Uajemi. Dario alikusanya jeshi alilotuma kuelekea Athens. Lakini katika Mapigano ya Marathon askari wa Athens pamoja na vikosi kutoka Sparta na miji mingine ya Wagiriki walishinda jeshi la Uajemi.

Dario aliandaa jeshi kubwa zaidi kwa uvamizi wa pili wa Ugiriki lakini alifariki kwenye mwezi wa Oktoba 486 KK. Alizikwa karibu na Persepolis katika kaburi lililokatwa katika mwamba wa mlima, mahali panapoitwa leo Naqsh-e Rostam. Alifuatwa na mwanawe Xerxes.

Kiasi cha kodi katika majimbo ya Milki ya Uajemi chini ya Waakhameni

Dario aligawa milki yake kwa majimbo yaliyoitwa "satrapia" na kila moja lilitawaliwa na gavana aliyeitwa "satrapi". Waliteuliwa na mfalme mwenyewe, wengi wao walikuwa Waajemi kutoka familia za wakubwa. Magavana waliwajibika kutunza sheria na utulivu, kuadhibu waasi na kukusanya kodi.

Taarifa zao zilipokelewa katika ofisi za kifalme huko Babeli, Persepolis na Shushani. Miji mikuu rasmi ya wafalme ilikuwa Persepolis, Pasargadae, Shushani na Ekbatana. Lugha rasmi ya kiutawala ilikuwa Kiaramu.

Dario aliimarisha uchumi kwa kuanzisha sarafu zilizosanifishwa; sarafu ya dhahabu ya gramu 8.4 ilitolewa iliyogawiwa kwa sarafu 20 za fedha (ajenti).

Aliagiza kujengwa kwa barabara ya kifalme kutoka Sardis katika Lydia kuvukia Anatolia hadi Mesopotamia ilipopita Ashuru na Babeli na kuishia Shushani, pamoja na barabara nyingine. Kwenye magharibi kulikuwa na daraja juu ya mlangobahari wa Bosporus. Huko Misri Dario aliagiza kukamilisha mfereji kati ya Bahari ya Shamu hadi Mto Nile.

Dario aliimarisha pia mfumo wa posta ulioanzishwa na Koreishi Mkuu. Kwenye njia kuu vituo vilijengwa vyenye matarishi na farasi. Barua kutoka ofisi ya mfalme au kutoka magavana zilipelekwa haraka hadi kituo kilichofuata ambako tarishi mwingine mwenye farasi aliipokea na kuendelea nayo. Herodoti aliandika kwamba njia kutoka Sardis hadi Shushani ilipitiwa katika siku tisa kwa matarishi hao ilhali safari ya kawaida ilidumu siku 90.

  1. DPh, four tablets from Persepolis
  2. Shahbazi, Shapur (1994), "Darius I the Great", Encyclopedia Iranica, vol. 7, New York: Columbia University, pp. 41–50
  3. Herodoti anamtaja kama "mbeba mkuki"; walinzi wa mfalme walibeba mkuki (Herodoti, Historia III.139)
  4. BEHISTUN Inscription - Persia, tovuti ya atlantisonline, iliangaliwa Agosti 2022
  5. Linganisha T. Cuyler Young, The consolidation of the empire and its limits of growth under Darius and Xerxes, The Cambridge Ancient History, vol 4, kurasa 43 ff, 8https://books.google.de/books?id=nNDpPqeDjo0C&pg=PA76&redir_esc=y#v=onepage&q&f=false online hapa]

Kujisomea

[hariri | hariri chanzo]