iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: https://sw.wikipedia.org/wiki/Almagesti
Almagesti - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Almagesti

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Toleo la Almagesti kwa Kigiriki (Mathematike Sintaksis) la mwaka 1900
Mfumo wa Ulimwengu kufuatana na Ptolemaio
Mfumo wa Ptolemao jinsi ilivyofundishwa mnamo mwaka 1524 pale Uholanzi;
Dunia: iko katikati
zinafuata mizingo ya Lunae (Mwezi), Mercurii (Utaridi), Veneris (Zuhura), Solis (Jua),
halafu ya Martis (Mirihi), Iovis (Mshtarii) na Saturni (Zohali)
halafu Octavum Firmamentum (mbingu wa nane), halafu Nonum Coelum Cristalinum (mbingu wa tisa, wa kioo),
Coelum Empireum Habitaculum Dei et Omnium Electorum (Mbingu wa moto, mahali pa Mungu na wa wote waliochaguliwa naye

Almagesti ni jina la kitabu cha Klaudio Ptolemaio (100 - 170 BK) kinachoshika hitimisho ya elimu ya Wagiriki wa Kale kuhusu astronomia. Kilitungwa kwa Kigiriki na kuhifadhiwa kwa njia ya tafsiri kwa Kiarabu na baadaye kwa Kilatini ikawa msingi wa elimu yote kuhusu nyota kwa miaka 1,500 hadi karne ya 17 na wataalamu wote kati ya Wakristo wa Ulaya na Waislamu wa Mashariki ya Kati walifuata maelezo yake.

Jina

Ptolemaio alitumia jina la Kigiriki μαθηματικὴ σύνταξις mathematike sintaksis (hitimisho ya elimu, kutoka σύνταξις sintaksis (hitimisho) na μαθηματικός mathematikos (kuhusu elimu)). Nakala za baadaye ziliitwa "megiste sintaksis" kwa maana ya "hitimisho kuu" na nakala hizi zilikuwa msingi wa tafsiri kwa Kiarabu ambako neno la Kigiriki "megiste" lilandikwa kwa herufi za kiarabu kama المجستى al-majisti iliyokuwa "Al-magest" katika tafsiri za baadaye kwa Kilatini.

Yaliyomo

Almagesti ina sehemu au "vitabu" 13 ndani yake:

  • Kitabu 1: Maelezo kuhusu mfumo wa ulimwengu , ambako DUnia iko kwenye kitovu cha yote na sayari pamoja na Jua na nyota zinaizunguka
  • Kitabu 2: Misingi ya hisabati inayotumiwa na Ptolemaio kwa kukadiria mwendo wa magimba ya angani
  • Kitabu 3: Kuhusu mwendo wa Jua angani, muda wa mwaka na badiliko la ekwinoksi
  • Vitabu 4 + 5: Kuhusu mwendo wa Mwezi, paralaksi yake, ukubwa na umbali kati ya Dunia, Jua na Mwezi
  • Kitabu 6: Kuhusu kupatwa kwa Jua na kupatwa kwa Mwezi
  • Vitabu 7 + 8: Mienendo ya nyota, orodha ya makundinyota na nyota; humo alianzisha utaratibu wa kupanga nyota kufuatana na mwangaza unaoonekana, akitofautisha ngazi 6 za mwangaza
  • Vitabu 9–13: vinajadili mienendo ya sayari alizojua yaani zile zinazoonekana kwa macho matupu yaani Utaridi (Mercury), Zuhura (Venus), Mirihi (Mars), Mshtarii (Jupiter) na Zohali (Saturn)

Katika Almagesti Ptolemaio alitaja makundinyota 48 ambazo ni msingi wa makundinyota 88 za kisasa. Pamoja na makundinyota aliorodhesha nyota 1020 na kwa kila nyota aliongeza vipimo vilivyowezesha wasomaji wake kukuta kila nyota kwenye anga.[1] Leo hii watafiti huamini ya kwamba Ptolemaio mwenyewe alitumia orodha iliyowahi kutungwa miaka 300 kabla yake na Hipparchos pamoja na vipimo vyake. [2]

Mapokeo

Katika nyakati za Kale kitabu cha Ptolemaio kilikuwa hitimisho kuu ya elimu ya siku zile. Jinsi ilivyo na maandiko mengi ya kale kilinakiliwa kwa mkono maana hii ilikuwa njia ya pekee kabla ya ugunduzi wa uchapaji wa vitabu. Baada ya kuporomoka kwa Dola la Roma nakala zake zilipotea katika Ulaya. Lakini katika milki ya Uislamu vitabu vingi vya Wagiriki vilitafsiriwa kwa Kiarabu kuanzia karne ya 9. Upatikanaji kwa Almagesti kwa Kiarabu ulikuwa msingi kwa maendeleo ya astronomia katika himaya ya Uislamu wakati wa Karne za Kati. Katika karne ya 12 Almagesti ilitafsiriwa kutoka Kiarabu kwa Kilatini na hivyo kupatikana kwa vyuo vikuu vya kwanza katika Ulaya. Hapo kuna msingi kwa majina mengi ya Kiarabu kwa nyota yanayotumiwa kimataifa maana wataalamu wa Ulaya walipokea wakati ule elimu ya kale pamoja na utafiti mpya kutoka kwa Waislamu kwa lugha ya Kiarabu.

Katika karne ya 15 Waturuki walivamia mabaki ya ufalme wa Byzanti na hapo wataalamu wengi wa huko walikimbilia Ulaya ya magharibi wakibeba pia vitabu vya zamani. Hapo nakala za kitabu asilia cha Ptolemaio ilifika Italia ikatafsiriwa kutoka Kigiriki kwa Kilatini na kuboresha matoleo yaliyopatikana katika Ulaya.

Umuhimu wa Ptolemaio ulipungua haraka tangu ugunduzi wa darubini ulioleta mlipuko wa elimu ya astronomia. Mfumo wake wa ulimwengu ulitambuliwa kuwa na kosa la kimsingi katika kitabu "De Revolutionibus“ cha Nicolaus Copernicus aliyetambua ya kwamba Dunia si kitovu cha ulimwengu bali Dunia pamoja na sayari zinazunguka Jua. Hii ilithibitishwa baadaye na Galileo Galilei na Johannes Kepler.

Hata hivyo orodha ya makundinyota 48 ya Ptolemaio katika Almagesti imepokelewa katika orodha rasmi ya makundinyota 88 iliyotolewa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia na kuwa msingi wake.

Marejeo

  1. Ptolemy’s Almagest, tovuti ya Ian Ridpath "Star Tales", iliangaliwa Disemba 2017
  2. Pickering, The Southern Limits of the Ancient Star Catalog and the Commentary of Hipparchos, The International Journal of Scientific History, Vol. 12 2002 Sept ISSN 1041›5440,

Viungo vya Nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu: