iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.
iBet uBet web content aggregator. Adding the entire web to your favor.



Link to original content: http://sw.wikipedia.org/wiki/Askofu
Askofu - Wikipedia, kamusi elezo huru Nenda kwa yaliyomo

Askofu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha ya Timotheo, mmoja kati ya maaskofu wa kwanza, ilivyochorwa katika Nuremberg chronicles f 109v(1493).

Askofu ni mtu mwenye cheo cha juu katika Kanisa. Kwa kawaida huliongoza katika eneo la dayosisi (jimbo) akisimamia shirika au parokia nyingi.

Historia ya cheo hicho

[hariri | hariri chanzo]

Episkopos katika Agano Jipya

[hariri | hariri chanzo]

Neno la Kiswahili "askofu" limetokana na أسقف "uskufu" ambalo ni umbo la Kiarabu la neno la Kigiriki επισκοπος "episkopos". Neno hilo katika mazingira ya Wakristo wa kwanza lilitumika kumtaja mwangalizi au msimamizi wa shughuli mbalimbali serikalini, katika shirika za wananchi au penye ujenzi.

Maandiko ya kwanza ya Agano Jipya yanayotumia neno hili ni nyaraka za Mtume Paulo, ambaye anataja kazi hiyo katika Fil 1,1. Lakini hakuna "episkopos" katika 1Kor 12,28 inayoorodhesha vyeo na kazi mbalimbali. Hii imechukuliwa na wataalamu wengi kama dalili ya kwamba wakati huo kile cha "episkopos" hakikuwa bado cheo cha kawaida katika shirika zote.

1Tim 3,1-7 na Tit 1,7 zinataja "episkopos" lakini wengine hudhani ya kwamba nyaraka hizo zimeandikwa baada ya Paulo.

Katika Mdo 20,28 wazee au viongozi wa ushirika wa Efeso waitwa "episkopoi" kwa jumla.

Haya yote yanachukuliwa wa wataalamu wengi ya kuwa wakati wa uandishi wa Agano Jipya cheo cha "askofu" hakikuwa bado cheo maalumu. Lakini katika shirika kadhaa alipatikana tayari kiongozi aliyekuwa na cheo cha juu kuliko wazee.

Episkopos kama cheo

[hariri | hariri chanzo]

Neno episkopos linaonekana kama cheo katika maandishi ya mwisho wa karne I na mwanzo wa karne II kama vile waraka wa kwanza wa Klementi ambapo askofu aonekana kuwa kiongozi mkuu wa kanisa la mji fulani.

Katika uenezi wa Ukristo madaraka ya askofu yalipanuka. Kadiri makanisa yalivyoenea hata nje ya miji hadi mashambani askofu akawa kiongozi wa eneo, si wa mji tu.

Wakati ule ngazi za daraja zilionekana: Kanisa la mji au eneo likiongozwa na episkopos (askofu) akishauriana na "presbiteri" (kiasili: wazee; baadaye: makasisi) na kusaidiwa na mashemasi au madikoni.

Kanisa Katoliki na Waorthodoksi

[hariri | hariri chanzo]

Wakatoliki na Waorthodoksi wana daraja takatifu ya Askofu, ambaye kwa kawaida ni mkuu wa kanisa katika ngazi ya dayosisi. Askofu ni kama baba wa makasisi (mapadri) na waumini wengine katika eneo lake.

Maaskofu hukutana kwenye sinodi na kufanya maazimio kuhusu mambo ya Kanisa lote.

Maaskofu wa nchi au eneo kubwa wako pamoja chini ya usimamizi wa Patriarki au wa Askofu mkuu.

Katika Kanisa Katoliki askofu wa Roma ni mkuu wa Maaskofu wote na wa Kanisa lote duniani akitajwa kwa jina la Papa.

Mafundisho ya mlolongo wa mitume

[hariri | hariri chanzo]

Katika mapokeo hayo askofu hutazamwa kama mwandamizi wa Mitume wa Yesu. Katika mafundisho hayo Yesu Kristo mwenyewe aliwaweka mitume wake 12 kuwa viongozi wa Kanisa lote na kuwapa madaraka. Madaraka hayo yalitolewa na mitume kwa kuwawekea mikono kichwani waandamizi wao waliopata hivyo kuwa maaskofu wa kwanza baada yao, nao wakafanya hivyo kwa waandamizi wao.

Kwa namna hiyo kuna mlolongo wa kuwekeana mikono kati ya wanaopokea nafasi ya uaskofu kuanzia mitume na kila kizazi cha maaskofu hadi leo. Hivyo maaskofu ni kiungo kati ya Yesu na waumini wa leo.

Askofu kati ya Waprotestanti

[hariri | hariri chanzo]
Askofu Janani Luwum wa Kanisa la Anglikana la Uganda aliyeuawa na Idi Amin.

Baadhi ya madhehebu ya Uprotestanti, hasa ya Anglikana, Wamoravian na sehemu za Walutheri yanadai kuwa yameendeleza mlolongo wa mitume. Hiyo iliweza kutokea hasa katika nchi kama Uingereza na Uswidi ambako wakati wa matengenezo ya Kiprotestanti maaskofu Wakatoliki wa awali walihamia upande wa matengenezo na utaratibu wa kiaskofu uliweza kuendelea.

Pamoja na hayo, Kanisa Katoliki halikubali kwamba ilitokea hivyo kihistoria, au kwamba mtazamo wa Waprotestanti wa wakati huo kuhusu daraja takatifu na ekaristi ulitosha kushirikisha kweli mamlaka ya Mitume wa Yesu. Hivyo Kanisa hilo kwa jumla halitambui maaskofu wa Kiprotestanti kuwa na sakramenti ya daraja.

Upande wao, Waprotestanti wengi hawaoni umuhimu wa mlolongo wa kuwekewa mikono tangu wakati wa Mitume hadi leo: kwao muhimu zaidi ni uaminifu kwa imani ya Mitume.

Madhehebu mengine kadhaa ya Kiprotestanti yanatumika cheo cha askofu kuwa kiongozi katika Kanisa.

Kwa kawaida mamlaka yake ni ndogo kuliko ile ya maaskofu wa Kikatoliki na wa Kiorthodoksi, kutokana na mtazamo tofauti kuhusu Kanisa na sakramenti, ambao katika miaka ya mwisho imezidi kuwa tofauti kutokana na Waprotestanti wengi kukubali wanawake wapewe uaskofu na ukasisi, kinyume cha mapokeo na imani ya Wakatoliki na Waorthodoksi.

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Askofu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.