Chombo cha angani
Chombo cha angani ni chombo kwa ajili ya kusafiri katika anga-nje ya dunia yetu.
Vyombo vya anga vinaundwa kwa kazi nyingi pamoja na mawasiliano, kubeba vifaa vya kutazama dunia au hali ya hewa, kufanyia utafiti sayari nyingine au kusafirisha watu na mizigo.
Vyombo vingine vinaingia kwa muda mfupi tu juu ya angahewa bila kumaliza mzingo wa dunia. Vingine vinazunguka kwenye mzingo kwa muda mrefu hata miaka.
Chombo cha angani cha kwanza kilikuwa Sputnik 1 kilichorushwa na Umoja wa Kisovyeti mwaka 1957 na kuzunguka dunia kwa miezi 3. Kilifuatwa na chombo cha Marekani "Explorer 1" mwaka 1958.
Mtu wa kwanza kwenye anga-nje alikuwa Mrusi Yuri Gagarin aliyerushwa na Umoja wa Kisovyeti kwa chombo cha Vostok 1 tarehe 12 Aprili 1961 na kumaliza mzingo mmoja wa dunia.
Marekani ilifuata tarehe 5 Mei 1961 kwa kumpeleka mwanaanga Alan Shepard nje ya angahewa lakini bila kumaliza mzingo kamili. Mnamo Februari 1963 Mmarekani John Glenn alifaulu kutimiza mizingo 3 ya dunia.
Marekani iliendelea kuandaa safari ya kufika mwezini na kuwafikisha wanaanga Neil Armstrong na Buzz Aldrin mwezini tarehe 20 Julai 1969 kwa kutumia chombo Apollo 11.
Ilhali maandalizi ya safari za kupeleka watu anga-nje ni ghali sana bila kuleta faida kubwa kiuchumi au kisayansi, kuna mamia ya vyombo vya anga vinavyozunguka dunia na kutekeleza kazi muhimu. Hivi huitwa pia satelaiti zikifuata mwendo wa kudumu wa kuzunguka dunia au kukaa mahali pamoja angani juu ya uso wa dunia. Utabiri wa hali ya hewa hutegemea data na picha kutoka vyomboanga. Sehemu ya majadiliano kwa simu na sehemu kubwa ya picha za televisheni hupitia satelaiti, na vilevile data za teknolojia kama GPS.
Vyomboanga vingine kama vipimaanga vinapewa kazi ya upelelezi angani hasa kukaribia sayari, kukusanya data zao na kuzituma duniani. Habari nyingi juu ya sayari za mfumo wa jua letu zimepatikana kutokana na upimaji uliotekelezwa na vipimaanga hivi.